MATUMIZI YA DAWA
Matumizi ya dawa za dharura kuzuia mimba na mipira ya kiume yapungua Uingereza
Amri ya kutotoka nje imesababisha kupungua kwa mauzo ya vidonge vya kuzuia mimba ambazo hutumika mara tu baada ya kujamiiana maarufu kama (morning-after pills), utafiti umeonesha.
Takwimu zinaonesha mauzo yalipungua kwa asilimia 50 kuanzia Machi hadi Aprili, huku idadi ya wanaokwenda kuandikiwa dawa hiyo hospitali nchini Uingereza ikipungua kwa karibu asilimia 20.
Huduma ya ushauri wa masuala ya uzazi Uingereza, imesema takwimu hiyo inaonesha haja ya dawa hizo kuanza kuuzwa katika maduka ya jumla bila kuhitaji karatasi ya daktari.
Serikali imesema mabadiliko yoyote ya sheria lazima yafikie kiwango cha usalama kinachohitaji.
Tofauti na nchi zenye mfumo mwingine wa afya kama Afrika Mashariki ambapo dawa hizi za kuzuia mimba punde tu baada ya ngono hupatikana moja kwa moja katika maduka ya kuuza dawa, nchini Uingereza ni lazima upate karatasi ya daktari.
'Hofu ya mimba ambazo hazikupangiwa yaongezeka'
Uingereza, manunuzi ya dawa hiyo yalipungua sio tu kwa wanaokwenda kwa daktari kutafuta kibali bali hata mauzo ya kwenye mtandao kutoka dawa 38,553 Machi hadi 18,500 Aprili.
Idadi hiyo ilipanda kidogo Mei hadi 23,918.
Januari mwaka huu, jumla ya dawa hizo 6,865 zilinunuliwa, 5,094 kwa Machi na 4,099 zikanunuliwa Aprili.
Sio manunuzi ya dawa hizo tu bali hata manunuzi ya mipira ya kondomu kwa mwezi Aprili pia nayo yalipungua.
Chama cha wataalamu wa magonjwa ya wanawake kinataka Uingereza kuiga nchi nyingine za Ulaya na Marekani kwa kuondoa sheria ya kwamba ni lazima uwe na karatasi ya daktari ili kupata dawa hiyo na badala yake iwe inapatikana tu kwenye maduka ya jumla.
"Kuondoa vizuizi vya kupatikana kwa dawa hii kwa sasa hivi ni muhimu sana hasa kutokana na shinikizo la huduma za afya zinavyoendelezwa kutokana na janga la corona," amesema Dkt. Ed Morris, rais wa chama hicho.
"Itakua haki ikiwa wanawake na wasichana wataweza kupata dawa hii ya kuzia mimba punde tu wanapoihitaji bila kuwa na haja ya kumuona daktari kwanza, kwa sababu ni ya dharura."
Kitivo cha Afya ya Uzazi kimesema huduma za afya zimeathirika na janga la corona.
Aidha, idara ya ushauri wa njia za uzazi wa mpango imeonya madaktari kuacha kutoa huduma ya kuweka kitanzi ama dawa zinazoingizwa mwilini kwa mpangilio fulani yaani implants kama njia moja ya uzazi wa mpango ili kuzia maambukizi ya virusi vya corona.
'Uwezekano wa kuathirika'
Deborah Evans, mwanafamasia huko Winchester anasema: "Bila shaka matumizi ya dawa hizo yamepungua na pengine hilo limechagiwa na kupungua kwa hamu ya kufanya mapenzi.
"Wanaotaka dawa za dharura za kuzuia mimba idadi yao imepungua pakubwa hata katika chuo chetu kikuu kwasababu wanafunzi wapo nyumbani.
"Lakini kwa wale wanandoa waliopatikana na kanuni ya kusalia ndani, nina wasiwasi kwamba wengine hawatafuti usaidizi na kuamua kubeba mimba ambazo hawakuzipangia."

Comments
Post a Comment