UBAGUZI
Burnely yatiwa aibu kwa bango la ubaguzi wa rangi uwanjani
GETTY IMAGESBurnley wameaibika baada ya bango lililokuwa na maneno 'Maisha ya wazungu ni muhimu Burnley' kupeperushwa na ndege moja katika uwanja wa Etihad wakati wa mechi ya Jumatatu kati ya Burnely na Manchester City.
Ndege hiyo ilizunguka mara kadhaa juu ya uwanja baada ya mchuano huo kuanza ambapo City aliichabanga Burnley mabao 5 kwa nunge.
Awali, wachezaji wa Burnley na City na wafanyakazi walikuwa wamepiga goti kuunga mkono harakati za vuguvugu la Black Lives Matter.
"Mashabiki wa aina hiyo hawastahili kuwa uwanjani," Ben Mee ameiambia BBC Radio 5 Live.
Mlinzi Mee ameongeza: "Tumeaibishwa, Tumefadhaishwa.
"Ni wale mashabiki wetu kidogo - Najua ninazungumza kwa niaba ya mashabiki wetu wengi wanaojitenga na mambo kama haya.
"Bila shaka ilikuwa na athari kubwa kwetu baada ya kuona bango hilo likipeperushwa angani.
"Ni aibu kwetu kwamba jina la timu yetu lilikuwa kwenye bango lile, walijaribu kujumuisha maneno ya bango hilo na timu hii- halina uhusiano wowote na timu yetu."
Katika taarifa, Burnley imesema kwamba bango hilo "haliwawakilishi kwa namna yoyote ile" msimamo wa klabu hiyo na kwamba watashirikiana kikamilifu na mamlaka kutambua wanaohusika na kuchukua hatua stahiki".
"Burnley inashutumu vikali waliotekeleza kitendo hicho cha kuweka maneno ya chuki kwenye bango na kulipeperusha uwanjani kwa ndege," taarifa hiyo imeongeza.
"Tungependa kuweka wazi kwamba wanaohusika na kitendo hichi hawakaribishwi Turf Moor.
"Tunaomba msamaha wa dhati kwa Ligi ya Primia, kwa Manchester City na kwa wote wanaoshirikiana kupaza sauti za Black Lives Matter.
"Klabu hii inarekodi nzuri ya kushirikiana na watu wa jinsia yote, dini na imani zote kupitia mradi wake wa jamii ulipata tuzo na kupinga ubaguzi wa aina yoyote ile.
"Tunaungana na wenzetu kikamilifu katika Ligi ya Primia wanaounga mkono juhudi za Black Lives Matter, zinazoendana na michezo mingine ya Ligi ya Primia tangu kuanza kwa juhudi hizi, wachezaji wetu na wafanyakazi walipiga goti bila kushinikizwa na mtu wakati mechi kati yetu na Manchester City inaanza."
Timu zote Burnley na City zilikuwa zimevalia shati ambazo majina ya wachezaji yamebadilishwa kwa maneno 'Black Lives Matter'.
Comments
Post a Comment